Huyu Ndiye Mtu Anayeweza Kukusaidia Kutatua Changamoto Unazozipitia.
Mara nyingi binadamu tumekuwa tukilalamika kuhusu
ugumu wa maisha na changamoto kuzidi kuongezeka kadiri siku zinavyozidi kwenda.
Katika jamii zetu kuomba msaada ni jambo jema kabisa lakini tunachozingatia ni
wapi au kwa mtu wa aina gani tunaomba msaada. Kwa wale wenye imani katika dini
kila mmoja na dini yake huomba ili aweze kupata unafuu juu ya changamoto zinazomkabili.
Lakini hii haimaanishi kuwa changamoto zinakwisha, ukivuka changamoto moja bado inakuja nyingine na nyingine hivyo hivyo, ilimradi
maisha hayaishi changamoto. Na hii hutokea kwa watu wenye vipato vikubwa na
vidogo, rika tofauti tofauti kwa ufupi kila mmoja bila kujali hadhi,muonekano
au uwezo wake alionao changamoto humkabili.
Wakati huu huwa mgumu lakini ugumu huu hutegemea
aina ya mtu aliyepata changamoto. Kuna wengine wanaweza kupata changamoto ndogo
na kuwa na uwezo mkubwa wa kuzihimili lakini wengine wakawa na changamoto ndogo
lakini wakashindwa kuzikabili.
Ukubwa au dogo wa changamoto hutegemeana na hali ya
upokeaji wa changamoto husika kwa yule alipatwa na changamoto hiyo. Katika hali
ya kawaida hakuna kipimo cha kuonesha kuwa changamoto za aina Fulani ni ngumu
kuliko za aina nyingine, inategemea sana na aina ya mtu na muda changamoto hiyo
inapotokea.
Mara nyingi tunapokumbwa na mitihani hii ya maisha
huwa tunatamani tupate mfariji kama nilivyoelezea kwenye sehemu ya kwanza hapo
juu. Lakini ukweli ni kwamba hakuna mtu anayeweza kutusaidia kutatua changamoto
tulizonazo bali kitu tunachoweza kukipata ni ushauri ambao baadae wewe binafsi utachagua ni
maamuzi gani unahitaji kuyafanya.(Soma pia http://boreshamaisha.blogspot.com/2016/03/hadithi-ya-mwizi.html)
Kuomba ushauri ni jambo jema hutusaidia sana
kupunguza msongo wa mawazo kutokana na mitihani tunayopitia lakini kufikiri
kuwa kuna mtu atakupa mbinu zitakazo kuhakikishia mafanikio sio rahisi. Unaweza
kupata uzoefu wa namna mtu mwingine anavyokabili changamoto inayofana na yakwako
lakini ukipata uzoefu huo inabidi utambue kuwa wewe pia ni mtu tofauti na uwe
mbunifu wa kutumia uzoefu uliopewa vizuri ili kuweka mambo yako sawa. Hata
kama utatamani kutatua kwa njia ya imani ya dini yako bado kuna hatua za kawaida
kama binadamu utatakiwa kuzichukua ikiwa ni kufanya maamuzi ambayo yataleta
mabadiliko katika hali unayopitia.
Kwa hiyo mtu anayeweza kutatua changamoto unayopitia
ni wewe mwenyewe, na hao wanaokuzunguka watakupa msaada wa mawazo tu, kwani
hata wao wanachangamoto zao. Utulivu, hekima na busara ni mambo muhimu sana
katika kufanya maamuzi sahihi.
Mwandishi: Esther Ngulwa
Barua Pepe: estherngulwa87@gmail.com